Home Audio Alikiba atua Los Angeles kutengeneza video ya kupinga ujangili wa tembo

Alikiba atua Los Angeles kutengeneza video ya kupinga ujangili wa tembo

SHARE
Alikiba
akiwa jijini Los Angeles Marekani na wasanii pamoja na watu mbalimbali
walioshiriki kutengeneza video ya wimbo wa kupinga ujangili wa tembo
inayotarajiwa kutoka mwezi ujao. Video hiyo imeratibiwa na Wildaid na
kudhaminiwa na Swiss Air pamoja na Pembe Club.

Katika
kutimiza jukumu lake jipya kama balozi wa kimataifa wa Wildaid, shirika
la kimataifa la uhifadhi wanyamapori, mwanamuziki maarufu Mtanzania –
Alikiba amesafiri kuelekea jiji la Los Angeles nchini Marekani ili
kutengeneza video ya kupinga ujangili kwa tembo wa Tanzania
akishirikiana na baadhi ya watengeneza filamu maarufu wa Hollywood.
Video
hiyo ambayo imesimamiwa na mtengeneza filamu maarufu Kevin Donovan
itatoka mwezi ujao ikiwa ni sehemu ya kampeni iliyozinduliwa jijini Dar
es salaam mwaka huu kupinga ujangili wa kuua tembo ikijulikana kama
“Ujangili Unatuumiza Sote”.
Kampeni
hiyo ilizinduliwa kwa ushirikiano wa Wildaid na African Wildlife
Foundation, mashirika ya kimataifa ya uhifadhi wanyamapori na maliasili
ambayo yanafanya kazi pamoja kwenye mabara ya Afrika na Asia kupunguza
ununuzi wa bidhaa zitokanazo na pembe za ndovu na kuhamasisha umma juu
ya janga la ujangili. Wimbo wa Alikiba umelenga kuwalinda na kuwafurahia
Tembo, mnyama aliyeko kwenye hatari ya kutoweka.
Wimbo
huo mpya wenye lengo la kuhamasisha vijana katika kuwalinda na
kuwapenda tembo umetengenezwa na kurekodiwa na Brian Rumsey na
kusimamiwa na Oththan Burnside ambaye ameishafanya kazi na wasanii kama
Rihanna na Sean Paul.
“Sisi kama Watanzania tunatakiwa kujivunia wanyama hawa wazuri ambao
wanauwawa na majangili kila siku,” alisema Alikiba. Kampeni hii imelenga
kuhamasisha Watanzania kujivunia wanyamapori wetu na kupambana na wote
wanaoua tembo kila siku kwa ajili ya pembe zao.”
Mradi
huu umeratibiwa na Wildaid na kudhaminiwa na shirika la ndege la
SwissAir huku kampuni ya Pembe Club ya Los Angeles inayotengeneza vito
vya madini mbalimbali na kutumia faida yake kusaidia harakati za
uhifadhi wanyama pori ikidhamini onyesho la Alikiba lililofanyika mwisho
wa wiki kwenye jiji hilo ambapo jumla ya dola milioni 2.5 zilichangwa
na wahisani kusaidia jitihada za kupinga ujangili wa tembo.

USISAHAU KULIKE PAGE YETU YA FACEBOOK HAPA CHINI                                                                                        

SHARE