Home Audio Mbunge Amkaba Koo Msimamizi Wa Uchaguzi Akidai Hati Yake

Mbunge Amkaba Koo Msimamizi Wa Uchaguzi Akidai Hati Yake

SHARE

Ili kupata hati ya ushindi Mbunge Mteule wa jimbo la Serengeti Mkoa wa Mara Marwa Ryoba (Chadema)alilazimika kumkaba Msimamizi wa Uchaguzi jimbo hilo,baada ya kutomkabidhi hati yake ya ushindi.

Tukio hilo lililovuta umati mkubwa wa watu wakishinikiza msimamizi huyo atoe hati lililazimu polisi kupiga mabomu ya machozi ili kutawanya watu ambao walikuwa wamezunguka uzio wa ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji.
Kabla ya kutokea kwa tukio hilo Ryoba alilazimika kupiga kelele akiwataka wananchi waliokuwa wamezingira ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmasahuri hiyo wakisubiri mbunge wao akabidhiwe hati ,huku akidai kuwa kuna mkakati wa kumchakachua unaoongozwa na msimamizi wa uchaguzi Naomi Nnko.
“Toka saa 10 jioni mara baada ya kunitangaza msimamizi anapiga piga chenga kunipa hati ya ushindi,amekuwa na maneno mengi …mara njoo kesho,nawajua hawa toka mapema amekuwa na mjadala na dk Stephen Kebwe,nimelazimika kuomba wananchi kwa kuwa wao ndiyo wamenichagua,ni haki yao toka saa kumi hadi saa moja anazungusha tu na watu hawatoki bila mimi kupata hati”alisema.
Hata hivyo kutokana na kushindwa kutoa hati mapema hali ilichafuka na wananchi wakaanza kurushia mawe  askari polisi  wakalazimika kupiga mabomu ya machozi ,hata hivyo kundi lingine lilianza kupiga mawe ofisi ya Takukuru na wengine  ofisi ya idara ya fedha na kupasua kioo,msimamizi huyo alilazimika kuchapa hati na kumkabidhi mbunge.
Akizungumzia tukio hilo Msimamizi wa Uchaguzi huku akilalamika alisema alikabwa na kusukwa sukwa na mbunge huyo na kuwa yeye hakuna na sababu ya kumnyima hati bali hakuwa na funguo za ofisi.

“Jamani hivi kweli mtatuongoza kwa staili hii tutafika,mimi nimekabwa na mbunge nikaburuzwa kuwa nitoe hati,nimemweleza sina funguo lakini analazimisha,lazima tujenge misingi mizuri ya kuheshimiana kwa kuwa tutafanya kazi pamoja,”alisema.
Hata hivyo wakati wa makabidhiano ya hati msimamizi huyo hakutaka kupigwa picha na mbunge huyo kwa madai kuwa yeye haitaji picha,”sihitaji picha mimi”alisema huku anamkabidhi akiwa amekaa kwenye kiti.
Hata hivyo baadhi ya watendaji wa serikali  na wananchi walisema kuwa chanzo cha fujo huwa ni wasimamizi wenye maslahi binafsi na vyama ama wagombea na si polisi,kwa tukio hilo wananchi walikuwa tayari kwa lolote kwa kuwa walikubali kunyeshewa na mvua ili kuhakikisha mbunge wao anapata haki,na kulazimisha matumizi ya nguvu bila sababu za msingi.
Mwenyekiti wa Chadema wilaya Sang’uda Manawa alisema kuwa wasimamizi ni chanzo cha migogoro katika chaguzi hasa wanapoingiza mapenzi yao badala ya kuzingatia sheria,kwa kuwa kundi hilo lilikuwa tayari kwa lolote na huenda kungetokea tukio baya ili kulinda haki yao isiporwe.
Kuhusu matukio mengine ya uvunjifu wa amani jimboni polisi walisema hali ni shwari na kuwa walijitahidi kudhibiti vikundi vya watu waliokuwa wamejipanga kuvuruga uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Wakati huo huo wafanyabiashara waliokuwa wamefunga kazi zao kwa siku mbili wakihofia matukio mabaya kabla ya kutangazwa kwa matokeo wameendelea na kazi kama kawaida huku mji ukiwa shwari.

LIKE PAGE YETU YA FACEBOOK HAPA CHINI                                                                                      

SHARE