Home Audio
SHARE

Juma Mtanda

1:49 PM

No Comments

Pwani/Dar. Mwenyekiti wa DP,
Mchungaji Christopher Mtikila (65) amefariki dunia katika ajali ya gari
iliyotokea katika Kijiji cha Msolwa, Chalinze wilayani Bagamoyo.

Mtikila
alifariki dunia jana saa 11.45 alfajiri akitokea mkoani Njombe kurejea
Dar es Salaam kwa shughuli za kampeni baada ya gari aina ya Toyota
Corrolla alilokuwa akisafiria pamoja na wenzake watatu kuacha njia na
kupinduka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jafari Mohamed alisema ajali hiyo ilichangiwa na mwendokasi wa gari hilo.

Alisema
Mchungaji Mtikila alikuwa amekaa kiti cha mbele bila kufunga mkanda na
hivyo kusababisha arushwe nje ya kupitia kioo cha mbele na gari kumlalia
kifuani na kupoteza maisha papo hapo huku abiria wengine wawili na
dereva wakijeruhiwa.

Mwili wa marehemu na majeruhi walipelekwa
Hospitali ya Tumbi. Wengine waliojeruhiwa ni Mchungaji Patrick Mgaya
(57) na Ally Mohamed (42) wote wakazi wa Dar es Salaam na dereva wa gari
hilo, George Steven (31) mkazi wa Mbezi Beach aliyekuwa amekodiwa na
Mchungaji Mtikila.

Majeruhi asimulia
Akisimulia
ajali hiyo, Mchungaji Mgaya ambaye ni nduguye Mtikila alisema walikuwa
wakitokea Njombe ambako walifanya mkutano wa kampeni za ubunge na
madiwani Jumamosi.

Alisema dereva wa gari hilo alikuwa akiendesha mwendo mkali na licha ya kumsihi mara kadhaa, hakusikia.

Alisema
walipofika Msolwa, walipokuta lori limeegeshwa mbele yao upande wa
kulia: “Tulipofika maeneo hayo kuna gari ambalo tulikuwa tumeongozana
nalo, likatupita kwa kasi na baada ya dereva wetu kutaka kupita, kukawa
na lori jingine linakuja, akaamua kulikwepa na kwenda pembeni mwa
barabara,” alisema.

Alieleza kuwa baada ya gari lao kwenda
pembeni, lilikuta shimo lililosababisha kupinduka mara tatu, ndipo
Mtikila alipotoka kupitia kioo cha mbele na gari likamlalia upande wa
kushoto kifuani.

“Mwili wake haukuwa na majeraha mbali na
kutokwa na damu kidogo mdomoni tu na baada ya hapo tulimtoa na muda
mfupi polisi walifika na kuchukua mwili wake,” alisema Mchungaji Mgaya.

Alisema
Mchungaji Mtikila alikuwa anataka wawahi kwa sababu alikuwa na mpango
wa kusafiri tena kwa ndege jana kwenda Musoma kuendelea na kampeni.

Eneo la ajali
Ajali
ilitokea katika eneo la wazi lenye mteremko mkali na lisilokuwa la
makazi ya watu. Kutokana na alama za gari hilo tangu lilipohama
barabarani na kuingia bondeni, inaonekana lilitembea umbali wa mita 100
na kisha kuruka juu na kugonga mti kabla ya kupinduka.

Kamanda
Mohamed alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mbali na mwendo kasi,
kuna uwezekano mkubwa pia dereva ambaye anashikiliwa na polisi kwa
mahojiano zaidi, alizidiwa na usingizi.

Rambirambi
Chama cha ACT- Wazalendo kimetuma salamu za rambirambi kikieleza kupokea kwa masikitiko kifo cha ghafla cha Mchungaji Mtikila.

Katika
taarifa yake, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba alitoa pole
kwa familia ya marehemu, ndugu jamaa na marafiki na Watanzania kwa
msiba huyo.

“ACT wazalendo inatambua mchango wa kina wa kutafuta
mageuzi ya kweli yaliyokuwa yakiendeshwa na Mchungaji Mtikila wakati wa
uhai wake. Tunaamini mchango wake kwa Taifa ulikuwa unahitajika kwa
kiasi kikubwa hasa wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu,” alisema
Mwigamba.CHANZO:MWANANCHI

SHARE