Home Audio BSS 2015: Kilichoficwa nyuma ya pazia chafichuka, Mshindi aibua gumzo

BSS 2015: Kilichoficwa nyuma ya pazia chafichuka, Mshindi aibua gumzo

SHARE

Na Musa Mateja na Imelda Mtema

MASHINDANO ya Bongo Star Search
(BSS) 2015, wikiendi iliyopita yalifikia tamati huku historia ya kwanza
ikiwekwa na kijana mwenye umri wa miaka 19 tu, Kayumba Juma aliyeibuka
kidedea kwa kuwatupa wenzake 6 waliofaulu kuingia fainali na licha ya
shughuli hiyo kumalizika salama, lakini kilichojificha nyuma ya pazia
kimefichuka.

Fainali hizo zilifanyika Oktoba 9, mwaka huu kwenye
Ukumbi wa King Solomon uliopo Ada Estate, Kinondoni jijini Dar huku
zikishuhudiwa na maelfu ya wakazi wa jiji, burudani zilikuwa kibao siku
hiyo ambapo zilianza saa 3: 30 usiku zikifunguliwa na mkali wa miondoko
ya R&B, Bongo, Bernard Paul ‘Ben Pol’.

WASHIRIKI WAANZA

Baada
ya Ben Pol kufungua ukurasa huo, kete ya kwanza kwa washiriki ilianza
kwa kumdondokea mshiriki kutoka Mwanza, Angel Mary Kato aliyeonesha
manjonjo yake akimpisha Kayumba Juma ambaye aliingia na Wimbo wa
Christian Bella huku akipata shangwe nyingi kutoka kwa mashabiki
waliomtunza fedha.

Baadaye, Nasibu Fonabo akichukua nafasi ya tatu
kwa kufungua jukwaa hilo, tena akitumia gitaa huku Kelvin Geryson
akiingia kwa makeke mengi na kumpisha Frida Amani ambaye alikuwa
mshiriki kutoka Kaskazini.
Jackline Kakengi kutoka Bukoba alitoka na kuacha washiriki wenzake wakisonga mbele na kuunda Tano Bora.

LAKINI SASA

Hata
hivyo, ukiachana na ushindi huo wa Kayumba, kuna mambo ambayo yalizua
gumzo ukumbini hapo ambapo u-team wa majaji. Wasanii waligawanywa katika
makundi ya Madam Ritha, Salama Jabir na Master J na kuonekana wazi hasa
pale mshiriki wa jaji mmojawapo alipokuwa akipongezwa tofauti na
ilivyokuwa kwa yule ambaye si wa timu yake, jambo lililolalamikiwa na
mashabiki.

Mashabiki wengi walisema, siku ya fainali, majaji hao
‘wanaojua kusema’ wangekuwa kimya kama inavyokuwa kwenye shindano la
Miss Tanzania.

MFANO NI SALAMA
Katika kipengele hicho cha
u-team, jaji Salama Jabir alionesha mapenzi yake waziwazi kwa Kayumba
baada ya kumsifia kutokana na kupafomu Wimbo wa Aisha Ramadhan ‘Isha
Mashauzi’ katika raundi ya mwisho.
Salama alisema: “Bwana wee gitaa
kitu gani? Sisi watu wa uswahilini bwana, tuna mambo yetu na hayo mambo
ya gitaa kwanza hatujayazoea, hongera Kayumba.” (akimaanisha kuwa,
Nasibu Fonabo hakufanya kitu baada ya kupafomu na gitaa).

MASHABIKI WASEMA KAYUMBA ALIANDALIWA

Baada
ya ushindi huo wa Kayumba, gumzo kubwa liliibuka mashabiki ukumbini
hapo wakidai kuwa aliandaliwa mapema kutwaa taji hilo kwa msimu huu
kwani baadhi ya kura zilionesha mapema.
“Bwana wee, yaani hapa ni
kama tumeliwa. Inaonesha kuwa nyuma ya pazia Kayumba aliandaliwa toka
kitambo awe mshindi kwani utaona hata majaji wenyewe, kama Salama
alionesha wazi mapenzi yake kwa mshiriki huyo,” alisema mmoja wa
wahudhuriaji.

KUNA UPENDELEO WA WANAUME?

Katika hatua
nyingine, baadhi ya mashabiki walisema mashindano hayo yametawaliwa na
uchaguzi wa wanaume tu licha ya muandaaji wake kuwa mwanamke.Walisema
mpaka juzi, BSS imetimiza misimu nane huku sita ikitwaliwa na wanaume
tu, jambo lililotafsiriwa kuwa huenda waandaaji wake hawazingatii usawa.

KUMBUKUMBU YA WIKIENDA

Ilibidi
gazeti hili lifukue kwenye kumbukumbu zake za nyuma na kubaini kwamba,
washiriki waliowahi kutwaa taji hilo tangu kuanzishwa mwaka 2006 ni
Jumanne Idd (mwanaume), Pascal Casian (mwanaume), Emmanuel Msuya
(mwanaume), Misoji Nkwabi (mwanamke), Walter Chilambo (mwanaume), Mariam
Ramadhan (mwanamke), Haji Ramadhan (mwanaume) na sasa Kayumba Juma
(mwanaume).

UKUMBI PIA WAZUA MANENO

Baadhi ya mashabiki
walisema kutokana na mashindano hayo kuwa makubwa, yangefanyiwa kwenye
ukumbi mkubwa zaidi kama ilivyozoeleka kuliko kupeleka sehemu ngeni.

MADAM NA GAUNI LA BEI MBAYA
Lingine lililozua gumzo ukumbini, ni Madam Ritha kuvaa gauni ambalo lilikadiriwa kuuzwa dukani kwa shilingi laki tano.

Ijumaa Wikienda lililazimika kumfuata Madam kwa lengo la kujua bei
ambapo alisema alilitungua dukani kwa shilingi milioni moja na laki nane
(1,800,000).

Mshindi wa Shindano la Bongo Star
Search 2015 (BSS), Kayumba Juma (katika), akiwa ameshikilia fedha zake
muda mfupi baada ya kuibuka kidedea kwenye fainali hizo zilizokuwa
zikifanyika usiku wa kuamkia leo katika Ukumbi wa King Solomoni uliopo
Namanga jijini Dar es Salaa.Jaji Mkuu wa mashindano hayo, Madam Rita (wa pili kutoka kushoto), akimtangaza mshindi huyo.Washiriki waliongia kwenye 6 bora ya mashindano hayo wakiwa jukwaani kabla ya mchujo huo kuanza.
Mmoja
wa Majaji wa shindano hilo (kulia), Master Jay akiingia ukumbini hapo
huku akiwa ameongozana na mpenzi wake ambaye ni msanii wa Bongo fleva
Shaa.
Majaji wakiwa kwenye meza yao ya kuratibia mashindano hayo.
Peter Msechu akiwa katika pozi kwenye Red Carpet.
Wasnii wanaounga kundi la Navy Kenzo wakipagawisha jukwaani hapo.
Msanii kutoka nchini Nigeria, Run Town anayetamba na kibao chake cha Gallardo, akipagawisha jukwaani hapo.
Mmoja wa washiriki waliokuwa wakichuana jukwaani hapo, Angel Marykato akisaka milioni 50.
Vijana wanaounda kundi la Yamoto Bendi wakitoa burudani kwenye fainali hizo.
Msanii wa Dansi Christiani Bella akitunza na mashabiki wake wakati akitumbuiza kwenye fainali hizo.
Bosi anayesimamia lebo ya Mkubwa na Wanawe, Saidi Fella akishuhudia kwa makini fainali hizo.
Mshiriki wa Shindano hilo kutoka Arusha, Frida Amani akipagawisha jukwaani hapo kuwania kitita cha shilingi milioni 50.Kala Jeremiah akikumbushia enzi zake katika mashindano hayo.
Msanii wa Bongo Fleva, Estelina Sanga ‘Linah’ akiwa katika pozi kwenye red Carpet ya mashindano hayo.Ben Poul akiwa katika pozi na mmoja wa mashabiki zake.
Baadhi ya washiriki waliyotolewa mapema kwenye kinyang’anyiro hicho wakihojiwa muda mfupi baada ya kuwasili ukumbini hapo.
Msanii wa Filamu, Muna Alphonce akiwa katika ubora wake kwenye tamasha hilo.
Kayumba akitunzwa na mashabiki wake kabla ya kutangazwa kuwa mshindi.
Madam Rita akifuta machozi muda mfupi baada ya kumkabidhi mshindi kitita cha shilingi milioni 50.
Madam Rita akiwa kwenye pozi.
Mmoja ya kikundi cha kudansi kikitumbuiza jukwaani hapo.
Mpiga picha wa Mtandao huu, Musa Mateja (kushoto), akihojiwa mara baada ya kuingia ukumbini hapo.
Baadhi ya mashabiki waliohudhuria ukumbini hapo wakifuatilia burudani hizo kwa makini.
SHARE