Home Audio UFAFANUZI KUTOKA REDET KUHUSU TAKWIMU ILIYOTOLEWA NA BAADHI YA VYOMBO VYA HABARI

UFAFANUZI KUTOKA REDET KUHUSU TAKWIMU ILIYOTOLEWA NA BAADHI YA VYOMBO VYA HABARI

SHARE

Baadhi
ya vyombo vya habari katika taarifa zao zilizochapishwa katika matoleo
yao ya Jumatatu tarehe 6 Julai, 2015 vimechapisha taarifa zinazohusu
utafiti uliofanywa na REDET juu ya Maoni ya Wananchi Kuhusu Uchaguzi
Mkuu Utakaofanyika Oktoba 2015. Taarifa hizi

zimesababisha wadau wengi
hapa nchini kutaka ufafanuzi kutoka REDET. Kama ilivyo kawaida yake
REDET imejijengea heshima na utamaduni wa kufanya kazi zake kwa misingi
ya uwazi na ukweli. Kwa hali hii tunapenda kutoa ufafanuzi kama
ifuatavyo:
i.
REDET ilifanya utafiti juu ya maoni ya wananchi kuhusu hali ya siasa
Tanzania na uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2015 kuanzia
tarehe 23 hadi 26 Juni 2015. Utafiti ulikusudiwa kufanyika katika mikoa
yote 30 Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa bahati mbaya kibali cha kufanya
utafiti Zanzibar hakikutolewa kwa wakati. Hivyo taarifa za utafiti
zilipatikana kutoka mikoa 25 ya Tanzania Bara tu. Badala ya kupokea
taarifa za mahojiano 1,500, zilipokelewa 1,250 sawa na takribian
asilimia 83. Rasimu ya taarifa ya awali iliandaliwa kutoka mikoa hiyo
tu;
ii.
Tarehe 2 Julai, 2015 REDET ilitoa mwaliko wa Mkutano wa Wanahabari ili
kuwawezesha Watanzania kupitia vyombo vya habari kupokea matokeo ya
utafiti Jumapili tarehe 5 Julai, 2015 saa 5.00 asubuhi;
iii.
Baada ya kutafakari kwa kina na kwa kuzingatia ukweli kwamba rasimu ya
taarifa ya utafiti haikuhusisha mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Uongozi wa REDET uliazimia kufanya juhudi zaidi ili kuwezesha
mamlaka husika katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuridhia utafiti
huu uhusishe pia mikoa ya Zanzibar, ili ripoti itakayotolewa iwe
kamilifu na yenye sura ya Kitaifa;
iv.
Tarehe 4 Julai, 2015, REDET ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu
kuhairishwa kwa mkutano wa wanahabari uliokuwa ufanyike tarehe 5 Julai,
2015 kutokana na kutokamilika kwa taarifa kamili ya utafiti;
v.
REDET imewasilisha maombi kwa uongozi wa juu wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kuomba uwasiliane na mamlaka husika Zanzibar ili ruhusa iweze
kutolewa kufanya utafiti huu katika mikoa mitano ya Zanzibar;
vi.
REDET itatoa taarifa kamili ya utafiti kuhusu Maoni ya Wananchi Kuhusu
Uchaguzi Mkuu Utakaofanyika Oktoba 2015, mara tu taarifa yake
itakapokamilika; na
vii. Mwisho, uongozi wa REDET unaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza.
Imetolewa na:
Menejimenti, Mpango wa Utafiti

 na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET).
SHARE