Home Audio TANZIA: Msanii wa muziki wa Dansi, Banza Stone(Ramadhani Masanja) afariki Dunia

TANZIA: Msanii wa muziki wa Dansi, Banza Stone(Ramadhani Masanja) afariki Dunia

SHARE

Banza Stone enzi za Uhai wake.
Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi, Banza Stone amefariki dunia leo
hii Ijumaa. Ramadhani Masanja amefikwa na umauti kutokana na kuandamwa
muda mrefu na magonjwa

Banza Stone (wa kwanza kulia) akiwa na Bendi ya Muziki Ya Twanga Pepeta

Shabani Ally Masanja ambae ni kaka wa Banza amethibitisha
kutokea kifo cha Banza Stone nyumbani Sinza na msiba uko Sinza njia
panda ya Lion. Banza Stone alikuwa anaugua ugonjwa wa fungus ya kichwa
na kifua.

Banza Stone aliyezaliwa mwaka 1972 na kufanikiwa kumaliza elimu ya
msingi katika shule ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam mwaka 1987,
alianza taratibu kujihusisha na masuala ya muziki akiwa angali mdogo.
Banza alianza muziki miaka 25 iliyopita, mara tu baada ya kumaliza elimu
yake ya msingi kwa kujihusisha na muziki wa Hip Hop, enzi hizo walikuwa
wakisikiliza katika redio. Wakati huo alikuwa na wenzake kama kina K
One na Scoz Man.

Wazazi wake waliweka pingamizi baada ya kuonekana muziki huo kuwa wa
kihuni na mwaka 1990 akaamua kuanza mchakato mpya wa kuwa mcheza dansi,
alicheza dansi kwenye maharusi na kufanikiwa kupata fedha kidogo. Banza
aliamua kwenda shule kusomea masuala ya mziki kwenye chuo cha utamaduni
cha Korea, Korea Cultural Music Centre mwaka 1990 mpaka 1991.

Baada ya kuhitimu cheti alianza kuimba katika bendi mbalimbali ikiwamo
The Heart Strings, Twiga Band, Achigo Band kama mpiga ngoma, Afri-Swez
na bendi nyingine ndogo ndogo. Alikuwa akidumu katika bendi kwa miezi
kadhaa, kabla ya kuhamia katika bendi nyingine mpaka alipoingia katika
bendi ya The African Stars, Twanga Pepeta na kuijenga bendi hiyo
barabara.

Alijiunga na chuo cha Sanaa Bagamoyo mwaka 2000 ambapo alipata mafunzo
kwa miaka miwili, alipomaliza alitoka Twanga Pepeta na kwenda Tanzania
One Theatre (TOT) na huko alijulikana zaidi kwa jina la Mwalimu wa
Walimu japo hakukaa sana na kuamua kuanzisha bendi yake iliyokuwa
ikiitwa Bambino Sound ambayo ilidumu kwa miezi kadhaa tu lakini
ilivunjika kutokana na kutokuwa na uongozi mzuri na akarudi African
stars Band na baadae kuhamia Extra Bongo.

Katika kipindi cha miaka 24 tangu aanze muziki wa dansi rasmi haikuwa
rahisi kwake kupata mafanikio, kwani alizunguka sana mpaka kuifikia
bendi ya The African Stars Twanga Pepeta mwaka 1995. Banza Stone
alipitia zaidi ya bendi tisa ikiwemo Rufita Band. Mwaka juzi msanii wa
muziki wa kizazi kipya, Hamisi Ramadhani H-Baba aliamua kumshirikisha
Banza kurekodi wimbo wake mpya wa Sina Raha.

Banza Stone amewahi kutamba na nyimbo kadhaa zikiwemo: Mtaji wa Maskini,
Kumekucha, Elimu ya Mjinga, Angurumapo Simba Mcheza Nani na Falsafa ya
Maisha. Amewahi pia kuimba vibao kadhaa vya taarabu ukiwamo Kuzaliwa
Mjini na ule wa Play Boy.

SHARE