Home Audio KUELEKEA ALL AFRICAN GAMES, TWIGA STARS INATIA HURUMA

KUELEKEA ALL AFRICAN GAMES, TWIGA STARS INATIA HURUMA

SHARE
Timu ya taifa ya wanawake Tanzania, maarufu Twiga Stars
inatarajia kuanza michuano ya All African games mwezi Septemba mwaka
huu.

Twiga Stars inatarajia kuanza michuano hiyo dhidi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo mwezi huo wa septemba.
Timu hiyo ya Twiga Stars iliyopo chini ya kocha Logatian
Kaijage ni miongoni mwa timu kumi bora barani Afrika kutokana na viwango
vya soka vya siku kadhaa zilizopita vya FIFA ya soka la wanawake.
Lakini kuelekea katika mashindano haya ya All African games,
napata wasiwasi hasa wa jitihada za shirikisho la soka Tanzania, TFF
kuiwezesha Twiga Stars.
Taarifa zilizopo ni kwamba Twiga Stars itaanza kambi ya
kujiandaa na michuano hii mwanzoni mwa mwezi huu wa Julai, ni sawa
lakini ushindi wa timu ni zaidi ya kuweka kambi miezi miwili. Nimesema
nina tia shaka jitihada zinazooneshwa na chombo chenye dhamana ya
kuiwezesha timu hii yaani TFF kwa kua hadi sasa sijasikia lolote toka
kwa shirikisho hilo kama tulivyozoea kwa timu ya wanaume, na hilo
linapunguza morali kwa wanadada hawa ambao wamewahi kutuwakilisha vizuri
kuliko hata wanaume katika michuano ya kimataifa.
Naunga mkono muda wa kambi uliowekwa kimsingi unatosheleza,
lakini shida hapa inakuja kwamba tulihitaji mechi nyingi za kirafiki ili
kuwapa uzoefu na umakini dada zetu hasa katika hatua kubwa kama hii.
Timu nyingi zinazoenda shiriki michuano hii zilikuwepo katika
michuano ya kombe la dunia la FIFA la wanawake na hapa ndio napata
shida kuamini, tunaweza kupata chochote katika michuano hii ya All
African games.
Timu hizi zilizotoka katika fainali za kombe la dunia hivi
karibuni, kiufundi ziko vizuri zaidi ya timu yetu ambayo husahaulika
hadi tunapopata mashindano.
Maandalizi ya ‘zima moto’ ambayo tumeyazoea kuona mara kadhaa
timu hii inaenda katika mashindano yanakatisha tamaa hasa kwa
watanzania wanaoipenda timu yao lakini pia kwa wachezaji wetu.
Wito wangu kwa wahusika ni kwamba, kama tunahitaji kushindana
na sio kushiriki, miezi miwili inatosha kwa kambi ya mwezi mmoja na
mwezi wa mwisho tunaweza pata mechi angalau tatu ngumu za kutupa uzoefu
na kujiamini kwa wachezaji wanapoanza kuipeperusha bendera ya nchi.
Lakini pia TFF wanatakiwa kuwa na ligi thabiti za akina dada
ili kuzidi kupata vipaji zaidi na kuwaimarisha waliopo na sio kutegemea
juhudi binafsi na kuibuka tu kwa wachezaji kutoka tusikokujua. Ligi bora
ya wanawake nchi nzima itazaa timu bora ya taifa la Tanzania.
Mwisho nitoe wito kwa wadau wote wa michezo nchini kutoegemea
tu kwa timu za taifa za wanaume pekee bali kuiangalia pia timu yetu ya
Twiga Stars ili kuwatia nguvu wafanye vizuri katika mashindano
wanayoiwakilisha nchi yetu.
SHARE